WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitawavumilia watu wote
wanaotumia vibaya fedha za umma ambazo zinapaswa kuleta maendeleo kwa
wananchi, zikiwemo na za Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi.
Amesema
mfuko huo unalenga kufanikisha ukusanyaji wa fedha za kutosha amabazo
ni muhimu kwa Taifa wakati huu tunapoazimia kumaliza ukimwi ifikapo
mwaka 2030..
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo leo (Jumanne, Novemba 28, 2017) wakati akifungua
kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani,
lililofanyika jijini Dar es Salaam.
“Nitoe
wito kwa Bodi ya Mfuko huu na watendaji wake kuhakikisha wanasimamia
kikamilifu fedha hizi ili ziweze kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa
Mfuko huu. “
Waziri
Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli
itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhamasisha wananchi, wadau na
sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kujenga nchi ya
viwanda ili waweze kufikia uchumi wa kati, jambo ambalo haliwezi
kufikiwa iwapo wananchi wake watakuwa hawana afya bora.
“Hatutaweza
kufikia malengo haya kama Taifa iwapo watu wetu hawatakuwa na afya bora
kwani nguvu kazi kwa ajili ya Tanzania ya Viwanda itatokana na wananchi
wenye nguvu na afya bora.”
“
Hivyo kama Serikali tutahakikisha tunaendelea kutoa huduma bora za afya
ili wananchi wetu waweze kuwa na afya bora. Tutaendelea kuwakinga
wananchi wetu hususan ni vijana ili Taifa letu liwe na nguvu kazi ya
kutosha hasa wakati huu tunapoanza mageuzi makubwa ya kiuchumi na
kimaendeleo.”
Pia
Waziri Mkuu amesema kwamba kwa sasa Watanzania wengi wana uelewa mkubwa
wa ukimwi lakini changamoto iliyopo ni kubadili tabia na kuachana na
tabia hatarishi zinazosababisha kupata maambukizo mapya.
Amesema
jambo hilo ni hatari kubwa kwa nchi yetu kwa sababu bado wananchi wengi
wanaendekeza tabia ya kuwa na wapenzi wengi tena kwa wakati mmoja na
hakuna uaminifu katika ndoa.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu “changia mfuko wa udhamini wa udhibiti ukimwi, okoa maisha”.
Kongamano
hilo lilihudhuliwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu-Walemavu Bibi Stella Ikupa Alex, Naibu Waziri Wizara ya Afya,
Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile,
Makamishna wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS).
Wengine
ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS),
Dkt Leonard maboko, Mwenyekiti wa Baraza la Wanaoishi na virusi vya
Ukimwi (NACOPHA), wawakilishi wa wadau wa maendeleo na wadau wa ukimwi
nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, NOVEMBA 28, 2017.
0 comments:
Post a Comment