Mwalimu
wa dini wa Kanisa Katoliki (katekista) Jimbo la Mpanda,mkoani Katavi
Noel Sitemele amefariki dunia muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza
ibada ya mazishi ya muumini wake yaliyofanyika katika makaburi ya
Mchakamchaka Kijiji cha Majalila wilayani Tanganyika mkoani Katavi.
Katekista
huyo alikuwa akitoa huduma ya kiroho katika Kigango cha Mchakamchaka
kilichopo katika Parokia ya Mpanda Ndogo katika Wilaya ya Tanganyika
mkoani Katavi.
Akizungumzia
mkasa huyo, Diwani wa Kata ya Mpanda Ndogo, Hamad Mapengo alisema licha
ya Sitemele kuwa mwalimu wa dini, katika uhai wake alikuwa pia
Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila kilichopo katika Halmashauri ya Mpanda
wilayani Tanganyika.
Mapengo
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda, alisema Katekista
alifariki dunia juzi saa 11 jioni muda mfupi baada ya kufikishwa
zahanati ya kijiji Majalila kutibiwa.
Alisema
kabla ya kukutwa na umauti, Katekista huyo alikuwa mwenye siha njema na
aliongoza ibada ya mazishi ya muumini wake hadi mwisho katika makaburi
ya Kigango cha Mchakamchaka kilichopo katika Kijiji cha Majalila ambapo
alianza kujisikia vibaya.
“Baada
ya kumaliza ibada hiyo ya mazishi, alianza kujisikia vibaya hivyo
akalazimika kurejea nyumbani kwake na kuwaacha waombolezaji makaburini,”
alieleza Mpaengo.
Alisema,
baada kufika nyumbani kwake, hali yake iliendelea kuwa mbaya na aliomba
msaada kutoka kwa majirani zake wamkimbize kwenye kituo cha afya kwa
matibabu.
Inaelezwa zahanati hiyo haiko mbali kutoka alikokuwa akiishi mwalimu huyo wa dini.
Mwenyekiti
alisema, taarifa za kifo cha Katekista huyo zilizagaa haraka kijijini
humo na kuwafikia waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu
aliyeongozewa ibada ya mazishi na Katekista huyo waliopata simanzi kubwa
wengine wakiwa hawaamini jambo hilo.
Maziko
yake yalifanyika jana makaburi ya kigango cha Mchakamchaka Kijiji cha
Majalila. Padri Paschal Kipenye wa Parokia ya Mpanda Ndogo aliongoza
ibada ya mazishi yaliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji akiwemo Mbunge
wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso.
IMEANDIKWA NA PETI SIYAME - HABARILEO
0 comments:
Post a Comment