Home » » Waliovunja kanisa na kuiba viti, vyombo vya muziki wakamatwa

Waliovunja kanisa na kuiba viti, vyombo vya muziki wakamatwa

Unknown | Wednesday, April 18, 2018 | 0 comments

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. 

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na Misako na Doria za mara kwa mara ili kudhibiti vitendo vya uhalifu pamoja na kuzuia matukio mbalimbali yakiwemo ya uporaji na ukabaji. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendesha Misako katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya baada ya kupata taarifa za uwepo wa vitendo vya uhalifu wa kuvunja Makanisa nyakati za usiku na kuiba mali mbalimbali zilizomo katika Makanisa. 

Misako hii ilianza mnamo tarehe 31.03.2018 na ilifanyika katika maeneo mbalimbali ndani ya Jiji la Mbeya na katika Wilaya ya Rungwe ilifanyika maeneo ya Kiwira na Wilaya ya Mbarali ilifanyika katika maeneo ya Igurusi.

Katika Misako hiyo, watuhumiwa watatu walikamatwa kutokana na kuhusika katika matukio ya uvunjaji na kuiba Makanisani nyakati mbalimbali. Watuhumiwa hao ni:-
  1.  WILLIAM SANKE [23] Mkazi wa Isanga
  2. ELIUDI MWANSULE [28] Mkazi wa Mwakibete Viwandani
  3. NOA MOLELA [26] Mkazi wa Mama John
Baada ya kukamatwa na kuhojiwa, watuhumiwa walikiri kuhusika katika matukio ya kuvunja na kuiba Makanisani nyakati mbalimbali na mara baada ya kuiba mali hizo huwapelekea wauzaji ambao pia wamekamatwa. 

Watuhumiwa hao ni:-
  1. HURUMA JOHN [52] Mkazi wa Igurusi Wilaya ya Mbarali
  2. HALID MWANGOKA [37] Mkazi wa Igurusi Wilaya ya Mbarali
  3. GODFREY MWALIMBA [28] Mkazi wa Mwakibete
  4.  GWAMAKA MWAIKAMBO [32] Mkazi wa Mwakibete
Baada ya kuhojiwa watuhumiwa wote walikiri kupokea mali hizo kutoka kwa mtuhumiwa WILLIAM SANKE na wenzake na baada ya kuzipokea huziuza kwa watu mbalimbali.

Misako hii imefanikisha kupatikana kwa mali mbalimbali za wizi ambazo ni:-
  1.     Spika kubwa 15 za aina mbalimbali
  2.     Mixer 08
  3.     Amplifier 01
  4.     Viti vya Plastic 108 vya rangi mbalimbali.
Watuhumiwa wote wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya na watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kupambana na wahalifu wanaojihusisha na dawa za kulevya. 

Kutokana na taarifa za kiintelijensia mnamo tarehe 11.04.2018 majira ya saa 17:00 jioni tuliweza kubaini kuwa huko maeneo ya Mlima James, Kiwanja kilichopimwa Plot Na.2590 Kitalu X Mwakibete, Kata ya Ilemi, Tarafa ya Sisimba, jiji na Mkoa wa Mbeya kuwa kuna wakulima ambao wanalima mazao mbalimbali kwa kuchanganya na miche ya Bhangi ipatayo 83.

Miche hiyo iling’olewa na wananchi wa eneo hilo kwa kushirikiana na viongozi wao wa Serikali za Mitaa chini ya usimamizi mkali wa Jeshi la Polisi. Jitihada za kumtafuta mhalifu wa tukio hili zinaendelea.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi MUSSA A. TAIBU anatoa wito kwa jamii kuachana na tamaa ya mali hasa kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu ili wapate mali na badala yake wafanye kazi halali. 

Aidha Kamanda TAIBU anaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukulia dhidi ya wahalifu. 

Pia Kamanda TAIBU anawasihi wananchi wa Mkoa wa Mbeya na Wilaya zake kuachana na tabia ya kilimo cha Bhangi kwani watakaokamatwa watahusika wenyewe katika kuteketeza mashamba hayo lakini pia sheria kali itachukuliwa dhidi yao.

Advertisement
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Copyright © 2018. AFRICAN NEWS BLOG - All Rights Reserved
Imetengenezwa na Edwin Moshi
Inaendeshwa na AFRICAN NEWS BLOG