RAIS
Mstaafu Benjamin Mkapa amewataka wadau mbalimbali na wananchi kuendelea
kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) kwa ajili ya
kukabiliana na ugonjwa huo nchini ambapo zaidi ya sh.milioni 200
zilipatikana.
Mkapa
alitoa ombi hilo wakati akiongoza harambee ya kuchangia mfuko huo
iliyofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa
na viongozi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya nje na ndani pamoja
na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
“Ni
wajibu kwa kila mwananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia mfuko
huu ili kusaidia mapambano ya Ukimwi hapa nchini na kuwa mapmbano hayo
si ya mtu mmoja” alisema Mkapa.
Katika hatua nyingine Rais Mstaafu Mkapa ameiomba Serikali kuendelea kutenga fedha za Ukimwi katika bajeti zake.
Akizungumza
katika harambee hiyo Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema kwamba Serikali itaendelea
kusimamia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) katika matumizi
ya fedha hizo.
Mhagama
alisema asilimia 60 ya fedha hizo zitatumika kununulia madawa, asilimia
25 itatumika katika kutoa huduma za kinga pamoja na kutoa elimu ya
kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi na asilimia 15 zitatumika kwa
ajili ya uwezeshaji na ufuatiliaji wa programu za Ukimwi.
Mhagama
aliongeza kuwa matumizi ya dawa za kufubaza VVU kwa wanawake ni
asilimia 92.9 wakati wanaume ni 86.1 na kuwa katika tisini ya tatu kati
ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15-64 ambao wametoa taarifa
kuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU asilimia 87.7 ya watu hao
inaonyesha kiasi cha VVU kimefubazwa wanawake ni asilimia 89.2 na
wanaume ni asilimia 84.
Alisema
utafiti huo pia umeonyesha kuwa maambukizo mapya ya VVU (HIV incidence)
kwa mwaka kwa watu wenye umri wa miaka 15-64 Tanzania Bara ni asilimia
0.29 ambayo ni sawa na watu 81,000.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Mfuko huo, Bw. Godfrey Simbeye alisema sekta binafsi imeunga
mkono kwa kiasi kikubwa katika kuchangia mfuko huo na kuwa hakutakuwa
na matumizi mabaya ya fedha hizo na zitakwenda kutumika kwa kile
kilichokusudiwa.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard
Maboko alimshukuru Rais Mstaafu Mkapa kwa kukubali kushiriki kuongoza
harambee hiyo na kueleza kuwa Tacaids imekuwa ikiendesha harambee
mbalimbali pamoja na kuandaa mashindano ya michezo na viingilio vyake
vimekuwa vikiingia katika mfuko huo.
0 comments:
Post a Comment