Maombi ya dhamana ya wabunge wawili wa Chadema na washtakiwa wengine 37 yamekwama kusikilizwa ikielezwa hakimu anaumwa.
Katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, imeelezwa hakimu Ivan Msack
anayesikiliza kesi hiyo ni mgonjwa hivyo imeahirishwa na washtakiwa
wamepelekwa rumande hadi Desemba 8,2017.
Akiahirisha
kesi hiyo leo Jumatano Desemba 6,2017, hakimu Erick Rwehumbiza amesema
Msack amepata maradhi ghafla na yuko hospitalini kwa matibabu.
Baada
ya kuelezwa mahakamani kuwa hakimu ni mgonjwa, upande wa utetezi
ulimuomba Rwehumbiza kesi hiyo ihamishiwe kwa hakimu mwingine.
Wakili
wa utetezi, Peter Kibatala amesema kuahirishwa kesi hiyo na kutotolewa
dhamana kwa washtakiwa kunalenga kuchelewesha upatikanaji wa haki.
Kibatala pia ameiomba Mahakama iruhusu wananchi kuingia ndani ya ukumbi kufuatilia uendeshaji wa kesi hiyo.
Wakili
wa Serikali, Sunday Hyera akizungumzia hoja ya wananchi kuruhusiwa
kuingia ndani ya ukumbi wa Mahakama amesema haina msingi katika kesi
hiyo na hakuna uwezekano wa kuiwasilisha mahakamani.
Hakimu Rwehumbiza akijibu hoja hizo, amesema alipewa jalada la kesi kwa ajili ya kuiahirisha.
Kuhusu
dhamana amesema ombi hilo litashughulikiwa na hakimu anayehusika na
iwapo hatakuwepo Desemba 8,2017 wataangalia namna ya kuihamishia kwa
hakimu mwingine.
Hakimu
Rwehumbiza amesema suala la wananchi kuingia mahakamani haliathiri
uendeshaji wa kesi kwa kuwa wanaweza kuwepo wawakilishi wao.
Wabunge
Susan Kiwanga wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero na washtakiwa
wengine walifikishwa mahakamani Novemba 30,2017 wakidaiwa Novemba
26,2017 katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi walifanya uharibifu wa
mali.
Wanadaiwa bila uhalali, huku wakijua wanatenda kosa walikula njama na kuchoma moto ofisi ya kata na kufanya uharibifu wa mali.
Hakimu
alisema angetoa uamuzi wa dhamana jana Desemba 5,2017 lakini hilo
halikufanyika kutokana na kuibuka hoja za kisheria kuhusu hati ya kiapo
ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo.
Kutokana
na mvutano wa kisheria, hakimu Msack aliahirisha kesi hiyo hadi leo
Jumatano Desemba 6,2017 ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja
kuhusu hati hiyo.

0 comments:
Post a Comment