Hali
ya taharuki na hofu imezuka katika kijiji cha Katani kata ya Nkandasi
wilayani Nkasi mkoani Rukwa na kusababisha waombolezaji kutimua mbio na
kuacha jeneza lenye mwili wa marehemu baada ya mvua kubwa kuanza
kunyesha ghafla yenye upepo na radi.
Tukio
hilo lilitokea hivi karibbuni majira ya saa 6 mchana baada ya kuanza kunyesha
mvua kubwa iliyoambatana na radi na upepo mkali ulioezua baadhi ya
nyumba za wananchi hao ambao walikuwa wakiomboleza msiba wa mwananchi
mwenzao aliyefariki baada ya kuugua siku chache zilizopita.
kwamujibu wa mashuhuda tukio hilo limezua hisia za kishirikina kwa wananchi wa kijiji hicho kwani miezi miwili iliyopita baba yake na marehemu huyo alifariki baada ya kugongwa na gari la kampuni ya ujenzi wa barabara na walipofanya maziko siku iliyofuata walikuta ngozi ya kondoo juu ya kaburi la marehemu kitendo kilicho washangaza wakazi hao.
Akizungumza
na wanahabari kwa nyakati tofauti mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Kaungo, Robert
Kanoni alisema wakiwa wanaelekea kufanya mazishi ya marehemu Dismas
Kanoni aliyefari juzi, ghafla mvua kubwa ilianza kunyesha hali
iliyosababisha baadhi ya waombolezaji kutimua mbio na kurejea majumbani
kutokana na hofu iliyoibuka kufuatia tukio hilo.
Alisema
baadhi ya wananchi walivumilia hali hiyo na kurudisha nyumbani jeneza
lililokuwa na mwili wa marehemu na kuahirisha maziko kwa muda ili
kupisha mvua hiyo na baadaye walikwenda kuzika katika makaburi yaliyopo
kijijini hapo.
Kanoni
alisema kutokana na mvua hiyo nyumba zipatazo 10 zimebomoka kabisa na
zinatakiwa kujengwa upya huku nyumba nyingine saba, zikiwa zimeezuliwa
paa na kuwaacha wakazi wake wakiwa hawana sehemu ya kukaa licha ya kuwa
wamepata hifadhi na misaada ya kibinaadamu kwa wenzao.
Naye
Peter Kalale mkazi wa kijiji hicho akizungumzia tukio hilo alisema mara
kwa mara kijiji hicho kimekuwa kikikumbwa na dhoruba pindi mvua
zinaponyesha kwakuwa kimepitiwa na mkondo wa upepo mkali ambao
unasababisha hali hiyo.
Alisema
changamoto iliyopo ni tabia ya wananchi kukata miti kwa ajili ya
mashamba na hivyo kusababisha pepo zinapovuma hazikuti kizuizi chochote
na hivyo imekuwa sababu ya kuezuliwa nyumba zao na hata kubomoka
kabisa.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya hiyo ambaye ni mkuu
wa wilaya hiyo Said Mtanda ilikiri kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito
kwa wananchi kujenga nyumba bora kwani miongoni mwa nyumba hizo zipo
ambazo zimeezekwa kwa nyasi.
Alisema
kuwa sera ya serikali ya awamu ya tano ni kuwahimiza wananchi wajenge
nyumba bora na za kisasa ili waweze kuepuka majanga yanayotokana na
tabia nchi kwani bila kufanya hivyo wananchi wataendelea kupata hasara.
Na Walter Mguluchuma
0 comments:
Post a Comment