Wakati
dunia ikielekea kuadhimisha siku ya UKIMWI kila ifikapo Desemba mosi ya
kila mwaka, bado Virusi Vya UKIMWI (VVU) na ugonjwa huo unabaki kuwa ni
changamoto muhimu ya kiafya ndani ya jamii hususani kwenye nchi zenye
kipato cha chini na kati.

Kutokana
na maendeleo yaliyofikiwa sasa katika upatikanaji wa tiba ya
mchanganyiko wa dawa zinazotumika kuzuia VVU kuongezeka mwilini
(antiretroviral therapy - ART), watu waliogundulika kuwa na VVU wanaishi
kwa muda mrefu na maisha yenye afya. Kwa kuongezea, imethibitishwa
kwamba dawa hizo zinazuia kuendelea kuongezeka kwa VVU.
Katika
kukupatia elimu zaidi juu ya ugonjwa huu, Jumia Travel ingependa
kukufahamisha juu ya mambo yafuatayo ambayo yamebainishwa na Shirika la
Afya Duniani (WHO), ambalo huunga mkono nchi mbalimbali katika kuunda na
kutekeleza sera na programu ili kuboresha na kuongeza jitihada za
kuzuia VVU, matibabu, huduma na kutoa msaada kwa watu wote wanaohitaji
msaada.

Taafirifa hizi zinatoa takwimu zilizopo sasa kuhusu ugonjwa huu pamoja na njia za kuuzia na kuutibu:
VVU
huambukiza seli za kwenye mfumo wa kinga za mwili. Maambukizi
husababisha kuendelea kuzorota kwa mfumo wa kinga ya mwili, huvunja
uwezo wa mwili kuweza kuepuka baadhi ya maambukizi na magonjwa. UKIMWI
hujulikana kuwa ni hatua ya juu kabisa ya VVU ambapo hujipambanua kwa
kujitokeza kwa maambukizi kati ya zaidi ya 20 au saratani zinahusiana na
virusi hivyo. 

VVU
vinaweza kuambukizwa kwa njia kadhaa. VVU vinaweza kuambukizwa kupitia:
kujihusisha na ngono isiyo salama; kuhamishiwa damu au bidhaa
inayohusiana na damu au kufanyiwa upandikizaji ambao sio salama;
kushirikiana kutumia vifaa vya kutobolea mwili (sindano) na vimiminika
au vya kuchorea michoro mwilini (tattoo); kutumia vifaa vya upasuaji na
vinginevyo vyenye ncha kali; na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto mchanga wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.
Zipo
njia kadhaa za kuzuia maambukizi ya VVU. Njia muhimu za kuzuia
maambukizi ya VVU ni: kufanya ngono salama kama vile kutumia kondomu;
kupima na kupatiwa matibabu kwa magonjwa yaliyoambukizwa kupitia ngono,
ikiwemo VVU ili kuzuia maambukizi kuendelea; hakikisha kwamba damu au
bidhaa yoyote inayohusiana na damu unayotaka kuitumia imepimwa VVU;
chagua njia salama ya kimatibabu wakati wa tohara endapo unatoka katika
nchi ambazo huchangia vifaa; kama una VVU anza mara moja kutumia dawa za
kusaidia kupunguza virusi kuongezeka mwilini kwa manufaa yako na pia
kuzuia kuambukiza VVU kwa mwenza au mtoto wako (kama ni mjamzito au
unanyonyesha).
Watu
milioni 36.7 duniani wanaishi na VVU. Duniani kote, inakadiriwa kuwa
watu milioni 36.7 (milioni 34.0 - 39.8) walikuwa wanaishi na VVU mwaka
2015, na kati ya hawa milioni 1.8 (milioni 1.5 - 2.0) walikuwa ni
watoto. Idadi kubwa ya watu wanaoishi na VVU wanapatikana kwenye nchi
zenye kipato cha chini na kati. Inakadiriwa watu milioni 2.1 (milioni
1.8 - 2.4) walipata maambukizi mapya ya VVU mwaka 2015. Inakadiriwa watu
milioni 35 mpaka sasa wamefariki kutokana na VVU, wakiwemo milioni 1.1
(940,000 mpaka milioni 1.3) mwaka 2015.
Mchanganyiko
wa dawa za ART huzuia virusi hivyo kuongezeka mwilini. Endapo kuzaliana
kwa VVU kukikoma, basi seli za kinga za mwili zitaweza kuishi kwa muda
mrefu na kuupatia mwili kinga dhidi ya maambukizi. Ufanisi wa dawa za
ART hupelekea kupungua kwa virusi, kiasi cha virusi mwilini, kwa kiasi
kikubwa hupunguza kuambukiza virusi kwa watu walio kwenye mahusiano ya
kimapenzi. Endapo mmojawapo wa wapenzi kwenye mahusiano anatumia dawa za
ART ipasavyo, kuna uwezekano wa maambukizi ya njia ya ngono kwa mwenza
ambaye hana VVU kupungua kwa kiasi cha takribani 96%. Kupanua wigo wa
matibabu ya VVU kunachangia katika jitihada za kuzuia VVU.
Katikati
ya mwaka 2016, watu milioni 18.2 duniani walipokea dawa za kusaidia
kuzuia VVU kuongezeka mwilini. Kati ya hawa zaidi ya milioni 16 wanaishi
kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati. Mwaka 2016, WHO ilitoa
toleo la pili la “Miongozo juu ya matumizi ya dawa za kusaidia kuzuia
kuongezeka VVU mwilini ili kutibu na kuzuia maambukizi ya VVU.” miongozo
hii imetoa mapendekezo kadhaa, ikiwemo pendekezo la kutoa dawa za
kusaidia kuzuia VVU kuongezeka mwilini kwa watoto kwa kipindi chote cha
maisha yao, vijana na watu wazima, wakiwemo wanawake wajawazito na
wanaonyonyesha waishio na VVU, licha ya idadi ya CD4 walizonazo mara
baada tu baada ya kugundulika. 

Kupima
VVU kunasaidia kuhakikisha matibabu kwa watu wenye uhitaji. Upatikanaji
wa huduma ya kupima VVU na madawa unatakiwa kuongezeka kwa kasi ili
kufikia lengo la kutokuwa na ugonjwa wa UKIMWI kufikia mwaka 2030.
Upimaji wa VVU bado ni mdogo, ambapo inakadiriwa kwamba 40% ya watu
wenye VVU au zaidi ya watu milioni 14 bado hawajatambulika na hawafahamu
hali ya maambukizi yao. WHO inapendekeza ubunifu kwenye mbinu za
kujipima wenyewe VVU na wenza wao ili kuongeza huduma za kupima VVU kwa
watu ambao hawajagundulika.
Inakadiriwa
watoto milioni 1.8 duniani wanaishi na VVU. Kwa mujibu wa takwimu za
mwaka 2015, wengi wa watoto hawa wanaishi katika nchi zilizopo kusini
mwa jangwa la Sahara na waliambukizwa kutoka kwa mama zao wenye VVU
wakati wa ujauzito, wakati wa kuzaliwa au kunyonyeshwa. Karibu watoto
150,000 (110,000 - 190,000) walipata maambukizi mapya ya VVU mwaka 2015.
Kuondoa
maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto inawezekana.
Ufikiwaji wa hatua za kuzuia maambukizi ya VVU umekuwa ni mdogo kwenye
nchi zenye kipato cha chini na kati. Lakini jitihada zimeendelea
kufanyika kwenye baadhi ya maeneo tofauti kama vile kuzuia maambukizi
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja na kuokoa maisha ya akina mama.
Mwaka 2015, karibu wajawazito 8 kati ya 10 wanaoishi na VVU au sawa na
wanawake milioni 1.1 walipokea dawa za kuzuia VVU kuongezeka mwilini.
Mwaka 2015, Cuba ilikuwa ni nchi ya kwanza kutangazwa na WHO kufanikiwa
kuzuia maambukizi ya VVU na Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mwaka 2016, nchi zingine tatu: Armenia, Belarus na Thailand nazo
zilithibitishwa kulifanikisha hilo.
VVU
ni sababu kubwa inayopelekea kupata ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB). Katika
mwaka 2015, inakadiriwa kuwa watu milioni 1.2 (11%) kati ya watu
milioni 10.4 duniani waliopata TB walikuwa ni waathirika wa VVU pia.
Mwaka huohuo takribani vifo 390,000 vilivyotokana na TB vilitokea
miongoni mwa watu waliokuwa wanaishi na VVU. Nchi za Kiafrika ambazo
zilizo chini ya WHO zilizidi karibu 75% ya idadi ya vifo vilivyokuwa
vinahusiana kati ya TB na VVU.
UKIMWI
ni janga ambalo linaikumba dunia nzima Tanzania ikiwemo, licha ya
ugonjwa huu kutzungumziwa kwenye kampeni tunazozisikia lakini ukweli ni
kwamba bado upo, ni tatizo, unaathiri na kuua nguvu kubwa ya taifa.
Katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani,
Jumia Travel ingependa kuikumbusha jamii inapaswa kutambua kwamba
jukumu la kuupiga vita ugonjwa huo bila ya kutegemea taasisi binafsi au
mashirika ya nje.
0 comments:
Post a Comment